Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro amesema utekelezaji wa Sheria ya Makubaliano ya Kukiri Makosa kwa Watuhumiwa (Plea Bargain) katika kipindi kilichopita ulikuwa na makosa ikiwemo Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuhodhi mamlaka yote ya kesi.
Akizungumza kupitia Power Breakfast ya CloudsFM, Waziri Ndumbaro amesema mapungufu mengine ni sheria kutomwangalia mwathirika ambaye anaweza kuwa amedhulumiwa mali zake lakini wakati wa majadiliano DPP anamalizana na mshtakiwa huku fedha zinazolipwa kwa Plea Bargain zikibaki Serikalini.
Kutokana na hayo, amesema Serikali imeandaa mabadiliko ya sheria yatakayoruhusu mahakimu na majaji kutoa hukumu zenye fidia kwa walalamikaji.
“Sasa hivi tunataka kuhakikisha kwamba hukumu hizi za Plea Bargain na hukumu nyingine zozote za jinai mwathirika aweze kunufaika moja kwa moja, kwa sasa hivi mpaka akafungue kesi za madai ama mahakama ikiamua vinginevyo,” amesema.
Serikali yafunga Wi-Fi ya bure maeneo ya umma
Aidha, amefafanua kuwa katika mchakato wa Plea Bargain watuhumiwa hawasamehewi ispokuwa wanapunguziwa adhabu kwa kuwa wanapunguza muda wa mahakama na Serikali wa kuendesha kesi, hivyo mtuhumiwa anapokiri kosa kwa hiari yake atahukumiwa kwa kulipa kiwango cha pesa ambacho kitakuwa kimekubalika.
“Lengo la Plea Bargain ni kwamba kupunguza watu watakaokuwa wanakaa magerezani. Kwa hiyo huyo mtu kwa maana ya kutiwa hatiani ametiwa hatiani ila kwa maaana ya adhabu, adhabu yake ni kulipa kiwango ambacho kitakuwa kimekubaliwa,” ameeleza.
Ndumbaro amesema mfumo huo unahusiana na makosa yote isipokuwa makosa makubwa kama mauaji, uhaini, ubakaji na ulawiti na siyo maamuzi ya DPP kuielekeza kesi kwenye mfumo huo ila mshatakiwa mwenyewe kwa kuandika barua kwa mkuu wa gereza endapo yupo gerezani au kwa DPP ikiwa yupo uraini.