Waziri Silaa: Wananchi wana wajibu wa kufahamu anwani zao za makazi
![](https://swahilitimes.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/WhatsApp-Image-2025-02-06-at-23.04.56.jpeg)
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa (Mb) amesema utekelezaji wa mfumo wa Anwani za Makazi nchini umelenga kurahisisha utoaji na upokeaji wa huduma mbalimbali ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Akizungumza jijini Dodoma katika hafla ya ufunguzi wa maadhimisho ya kwanza ya wiki ya Anwani za Makazi 2025, Waziri Silaa amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila nyumba, jengo, kiwanja, huduma, ofisi au eneo la biashara linatambulika kwa Anwani ya Makazi. Anwani ya Makazi inaundwa na Namba ya Anwani maarufu kama namba ya nyumba; Jina la Barabara au Mtaa; na Postikodi.
“ Mfumo wa Anwani za Makazi ni endelevu kwa sababu ya mabadiliko ya makazi, wakazi na huduma, hivyo kufanyika kwa maadhimisho haya kutaongeza hamasa kwa Taasisi za umma na binafsi pamoja na wananchi kuweza kutambua na kutumia Anwani za Makazi katika shughuli za kijamii na kiuchumi,” amesema.
Ameongeza kuwa “Wananchi wana wajibu wa kuzifahamu anwani zao za makazi na kuzitumia katika kujitambulisha, na iwapo watahitaji msaada au ufafanuzi wafike kwa watendaji wa Mitaa, Vijiji ama Shehia au kwa waratibu wa Mfumo wa Anwani za Makazi waliopo katika ofisi za Halmashauri.”
Maadhimisho ya Wiki ya Anwani za Makazi kwa mwaka 2025 yanaadhimishwa kwa mara ya kwanza tangu kukamilika kwa Operesheni Anwani ya Makazi iliyofanyika mwaka 2022 yakiwa na kauli mbiu inayosema “Tambua na tumia Anwani za Makazi kurahisisha utoaji na upokeaji huduma.”