Waziri Ulega akemea vitendo vya rushwa miongoni mwa watumishi wa TEMESA
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amekemea vitendo vya ubabaishaji na rushwa miongoni mwa watumishi wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) akisema vinaweza kufuta mazuri yote ambayo taasisi hiyo imekuwa ikiyafanya.
Akizungumza na Menejimenti ya TEMESA na Mameneja wa Mikoa jijini Dodoma, Waziri Ulega ameeleza Serikali imedhamiria kuifanya TEMESA kuwa taasisi namba moja na kimbilio la wote katika utengenezaji wa magari ya Serikali na binafsi.
“Tunatakiwa kupiga vita sana vitendo vya ubabaishaji na rushwa. Huu ndiyo ugonjwa unaoharibu taasisi nyingi na kwa kweli tunahitaji kutumia uwezo wetu wote kupambana na jambo hili,” amesema.
Ameongeza kuwa “Hongereni kwa kuanzisha mkakati wa mpya wa kufanya kazi utakaowawezesha kujiendesha kibiashara kwa kushirikiana na sekta binafsi pale inapobidi ili kuihudumia jamii kikamilifu. Sisi TEMESA ni lazima tuwaoneshe watu ukinilipa nitakufanyia kazi kwa wakati.”
Hata hivyo, amezipongeza Taasisi za BOT, EWURA, TANESCO na TRA kwa kulipa madeni yao kwa wakati na kupewa huduma kwa haraka na kuzitaka taasisi nyingine za Serikali kuweka mikataba ya huduma bora na za haraka na TEMESA ili kusaidia taasisi hiyo kuondokana na madeni.
Mbali na hilo, ameeleza kuwa zaidi ya Shilingi Bilioni 67.4 zimetumika katika miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kujenga vivuko vipya sita (6), ukarabati wa vivuko saba (7) na ujenzi wa miundombinu ya vivuko ambayo ni maegesho na majengo ya abiria katika Ziwa Victoria na Bahari ya Hindi.