
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amemuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi kuwasimamisha kazi wasimamizi wote wa mizani waliokuwa zamu katika mizani zilizopo katika barabara kuu ya T1 inayoanzia Dar es Salaam – Zambia kupitia mpaka wa Tunduma kwa ajili ya kupisha uchunguzi wa malalamiko katika mizani hizo.
Ulega amefanya maamuzi hayo mara baada ya kadhia iliyojitokeza hivi karibuni kwa msafirishaji Bi. Pamela James Bukumbi mwenye gari ya mizigo namba T 137 DLQ likiwa na tela T 567 CUR iliyotokea katika kituo cha mizani ya Vigwaza akilalamika kuhusu kutozwa faini ya kuzidisha uzito katika mizani hiyo wakati mizani nyingine alizopita gari yake haikuwa imezidisha uzito.
Ulega ametoa maelekezo hayo jijini Dodoma mara baada ya kupata taarifa hiyo na kusikiliza pande zote mbili kutoka kwa mlalamikaji na mlalamikiwa ambaye ni Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na kubaini kuwa lipo tatizo la wazi ambalo limesababisha kadhia hiyo na kutoa maelekezo makuu matano.
Ulega ameeleza kuwa tayari timu ya wataalam ya kuchunguza tukio hilo imeundwa ili kufuatilia safari nzima ya gari hilo ili kupata hali halisi na kuwasilisha mapendekezo mengine ili hatua za kinidhamu ziweze kuchukuliwa dhidi ya wale wote ambao watabainika na vitendo visivyoridhisha.
Aidha, Waziri Ulega ameiagiza TANROADS kuanza hatua za kubadilisha mifumo ya uendeshaji wa mizani 78 zote nchini haraka iwezekanavyo kwa kutangaza kwa watoa huduma wenye nia kuja na teknolojia ambazo ni ‘automated’ ili kupunguza muingiliano baina ya watu na watu na hivyo kumuwezesha dereva kujihudumia kwa kutumia mifumo jambo ambalo ni mkakati wa Wizara wa muda mrefu.