
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ameagiza mameneja na wasimamizi wa miradi ya ujenzi nchini kuacha tabia ya kuwafukuza kazi kiholela vijana walio kwenye miradi, badala yake hatua zichukuliwe kwa mujibu wa kanuni za kazi.
Agizo hilo limetolewa jijini Dar es Salaam wakati akikagua ujenzi wa miundombinu ya barabara Yaendayo Haraka Awamu ya Nne (BRT 4) sehemu ya Ubungo hadi Mwenge (km 13.5) ambapo amepokea changamoto za vijana wa kitanzania kufukuzwa kazi wanapolalamika au kutotendewa haki ikiwemo kucheleweshewa stahiki zao na Mkandarasi China-Geo Engineering Corporation anayetekeleza mradi huo.
Ulega amesisitiza kuwa kijana akifanya makosa au ukiukaji wa sheria, hatua zichukuliwe kwa mujibu wa kanuni za kazi, na kuiagiza TANROADS kufanya ufuatiliaji wa karibu kuhakikisha vijana wanafanya kazi katika mazingira salama na yenye haki.
Aidha, Waziri Ulega baada ya kukagua ujenzi wa barabara hiyo kipande cha Ubungo – Mwenge, ametoa miezi miwili kwa Mkandarasi China-Geo Engineering kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo kama mkataba unavyosema na sio vinginevyo.








