Waziri Ummy atoa miezi mitatu vifungashio vya plastiki kuondolewa sokoni

0
22

Serikali imetoa miezi mitatu kwa wenye shehena ya vifungashio visivyokidhi viwango vya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) vinaondolewa sokoni.

Agizo hilo limetolewa leo Januari 8, 2020 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Ummy Mwalimu wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Ofisi hiyo jijini Dodoma kuhusu matumizi ya vifungashio vya plastiki kutumika kama vibebeo vya bidhaa.

Ummy amesema kuwa pamoja na mafanikio yaliyopatikana kutokana na katazo la mifuko ya plastiki siku za hivi karibuni kumejitokeza changamoto ya matumizi ya vifungashio vya plastiki aina ya tubings visivyokuwa na sifa na hivyo kutokukidhi matakwa yaliyowekwa na TBS.

Aidha, Waziri Ummy aliongeza kuwa vifungashio hivi kwa sasa vinazalishwa kwa wingi na kwa ukubwa mbalimbali na vimekuwa vikitumika kama mifuko ya kubebea bidhaa sokoni na kuleta dhana kuwa mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku imerudi kivingine kama “vifungashio”.

Kwa mantiki hiyo Waziri Ummy amewataka wasambazaji, wazalishaji wa vifungashio hivi na waagizaji kuacha mara moja kuzalisha, kusambaza, kuuza na kutumia vifungashio hivyo na kusisitiza kuwa baada ya kipindi hicho Serikali haitatoa tangazo lingine lolote kuhusiana na katazo la matumizi ya vifungashio visivyokuwa na ubora.

Waziri huyo amesema Serikali itachukua hatua kali kwa mujibu kisheria na katika kipindi hiki wanaendelea na operesheni maalumu kuwabaini wanaokwamisha mafanikio haya kwa kuzalisha na kusambaza vifungashio hivyo na hatutawavumilia watu hawa.

“Napenda kuwakikishia wananchi kuwa Serikali kupitia TBS inayo kanzidata ya wazalishaji wa kutosha wa vifungashio vinavyokidhi viwango na hivyo hapatakuwa na uhaba wa vifungashio vinavyokidhi viwango baada ya kipindi hicho cha miezi mitatu.

Nitumie nafasi hii kuwaasa wazalishaji na wawekezaji wa ndani kuchangamkia fursa hii kwa kuzalisha vifungashio vyenye kukidhi viwango nilivyobainisha,” alisema.

Akizungumzia kuhusu katazo la mifuko ya plastiki Waziri Ummy alisema utekelezaji wa katazo hilo umefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kipindi chote cha mwaka mmoja na nusu tangu Serikali ilipotoa tangazo hilo.

Send this to a friend