Waziri Ummy: Kuna kila dalili kwamba UTI imekuwa sugu

0
43

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Serikali itafanya uchunguzi na matatibabu ya ugonjwa wa maambukizi katika njia ya mkojo (UTI) ambao bakteria wake wameonesha kustaimili dawa.

Ameyasema hayo jijini Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa baraza jipya lililoteuliwa la Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), na kueleza kuwa kutokana na idadi kubwa ya wanaopata huduma ya matibabu kubainika kuwa na UTI, kuna dalili kwamba ugonjwa huo umekuwa sugu kwa dawa au mfumo wake wa utambuzi haufai.

“Kuna kila dalili kwamba UTI inaweza kuwa sugu kwa Antimicrobial Resistant (AMR) kwa sababu karibu kila mgonjwa anayefika hospitalini kupata dawa hubainika mara kwa mara kuwa ana UTI, nadhani kuna dosari mahali,” amesema Waziri Ummy.

Ameongeza kuwa inawezekana UTI imetengeneza usugu, hivyo ameielekeza baraza jipya la NIMR kufanyia utafiti suala hilo na kuja na ushahidi wa kisayansi ili kuwezesha nchi kuona ukubwa wa tatizo hilo.

Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi, Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Profesa Yunus Mgaya amesema kutokana na uchunguzi wao kulikuwa na tatizo la utambuzi na matibabu ya UTI.

“Kwa namna vipimo vinavyochukuliwa, inawezekana watu wakatumia dawa nyingi za bakteria ambazo zinaweza kusababisha usugu wa dawa. Katika utafiti wetu tutakuja na muda gani unapaswa kuchukua kwa vipimo vya UTI kuleta matokeo,” amesema.

Naye Mtaalamu wa masuala ya afya ya jamii, Dkt. Faustine Ndugulile amesema jinsi magonjwa ya UTI na malaria yanavyofanyiwa uchunguzi nchini, ndiyo chanzo cha watu wengi kugundulika kuwa na magonjwa hayo.

“Ili kuwa na uhakika wa aina ya bakteria wanaosababisha UTI, utahitaji angalau saa 24 za kupima na saa nyingine 24 ili kubaini dawa maalum za kutibu bakteria hao,” amesema Ndugulile.
Chanzo: Mwananchi

Send this to a friend