Waziri Ummy Mwalimu: Corona inaweza kuambukizwa kwa njia ya hewa

0
47
Ummy Mwalimu

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema kuwa tafiti mpya zinaonesha kuwa virusi vya corona vinaweza kuambukizwa hata kwa njia ya hewa, na kwamba serikali itatoa muongozo kuhakikisha watu wanavaa barakoa (masks) wanapotoka makwao.

Ummy ameyasema hayo leo katika mkutano na viongozi wa dini ambao ulilenga kutoa elimu na kueleza hali ya maambukizi ya virusi vya corona hadi sasa nchini Tanzania, ambapo hadi sasa jumla ya visa 25 vimeripotiwa nchini.

“Tupo katika kipindi cha mlipuko na ugonjwa huu [COVID-19] unaambukiza, sasa hivi takwimu mpya zinaonesha hata kwa njia hewa, kwa hiyo wataalamu watatoa taarifa,” ameeleza Ummy.

Ameongeza kuwa, licha ya kwamba muongozo wa Shirika la Afya Duniani (WHO) unaelekeza kuwa wanaotakiwa kuvaa barakoa ni wagonjwa, wanaowahudumia wagonjwa, au waliopo kwenye maeneo hatarishi, lakini kutokana na uwezekano wa kuambukiza/kuambukizwa kwa njia ya hewa, serikali itatoa muongozo unaowataka wananchi wote kuvaa barakoa wanapotoa majumbani au kwenda kwenye maeneo yenye watu wengi.

Aidha, amewasihi viongozi wa dini kuwalelekeza waumini wao kuchukua tahadhari ya kujikinga na homa ya mapafu inayosababishwa na virusi hivyo kwa kuhakikisha wananawa mikono, wanakaa umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu, wanafunika mdomo wakipiga chafya au kukohoa.

Ameongeza kwamba, licha ya kuwepo kwa tamko la Rais Dkt Magufuli la kutokufunga nyumba za ibada, lakini ni muhimu kuhakikisha nyumba hizo hazijai watu, na ibada zinakuwa fupi ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Send this to a friend