Waziri Ummy: Wingi wa semina unachelewesha huduma kwa wananchi

0
14

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amewataka wataalamu wa afya nchini kupunguza semina ili kuwa na muda zaidi wa kutoa huduma bora za matibabu kwa wananchi.

Ameyasema hayo leo Julai 10, 2023 katika ziara yake mkoani Simiyu wakati akizungumza na viongozi wa Mkoa huo chini ya Mkuu wa Mkoa, Yahaya Nawanda.

“Wataalamu wa afya punguzeni semina maana mmekuwa na semina nyingi hadi kupelekea wagonjwa kukosa huduma kwa wakati na kumekuwa na msomgamano mkubwa katika vituo vya kutolea huduma za afya sababu ya semina”, amesema

Aidha, amesema utolewaji wa huduma za afya nchini hakuna kilichosimama kwa kuwa Serikali imejenga majengo ya hospitali, imetoa dawa na vifaa tiba, hivyo ni jukumu la wataalamu wa Afya kutoa huduma bora patika vituo hivyo.

Waziri Ummy atoa tamko kuhusu mtumishi aliyeosha vifaa vya hospitali kwa maji baridi

“Tunamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia kila kitu katika Sekta ya Afya ikiwemo majengo, vifaa tiba, kuajiri wataalamu na sasa ni jukumu letu wataalamu kutoa huduma bora kwa wananchi kwani ndio dhamira ya Serikali,” ameongeza.

Ameongeza kuwa, lengo la Serikali ni kutoa huduma bora za Afya kwa Watanzania na kwa mara ya kwanza Serikali imetoa hela za dawa kwa asilimia 100, hivyo amevitaka vituo vyote vya Afya kuwa na dawa zote muhimu ili kumsaidia mwananchi kupata huduma za matibabu kwa wakati.

Send this to a friend