Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Ikulu Zanzibar, Ali Suleiman amesema ili Tanzania iweze kufikia malengo ya maendeleo iliyojiwekea, lazima iwe na sera bora ya mambo ya nje inayozingatia maoni na matakwa ya makundi yote ya wadau nchini.
Amesema hayo katika Kongamano la wadau la kukusanya maoni kuhusu marekebisho ya Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 lililofanyika mjini Zanzibar likiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kushirikisha wananchi kutoa maoni.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba (Mb.) amesema Tanzania inaushawishi mkubwa duniani tofauti na nguvu zake za kiuchumi na kijeshi kutokana na kuwa na sera bora ya Mambo ya Nje, hivyo ili iendelee kuwa na ushawishi huo duniani lazima itungwe sera imara itakayozingatia maoni ya wadau wote.
Ameongeza kuwa Sera ya Mambo ya Nje ina uhusiano wa moja kwa moja na malengo ya maendeleo ya nchi, hivyo mchakato wa utungaji wa Sera ya Mambo ya Nje lazima ushirikishe wadau kwa kuwa maendeleo ni jambo linalomgusa kila mmoja.
Aidha, ametaja baadhi ya mambo yaliyosababisha Serikali kufanya marekebisho ya sera hiyo kuwa ni pamoja na mabadiliko ya tabianchi, uvumbuzi wa teknolojia mpya, kuibuka kwa wadau wapya wa maendeleo wenye nguvu na ushawishi.