Waziri wa Maji, Juma Aweso anusurika kutumbuliwa na Rais Magufuli

0
88

Rais Dkt. Maguful amesema kuwa endapo Waziri wa Maji, Juma Aweso asingewafukuza kazi wakandarasi wa mradi wa maji katika Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, basi yeye angelazimika kumfukuza kazi waziri huyo.

Dkt. Magufuli ametoa siri hiyo akizungumza na wakazi wa Shinyanga katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa Maji wa Kagongwa – Isaka ambao umegharamiwa na serikali kwa TZS bilioni 23.1.

“Nashukuru umeanza kuchukua hatua kwa wakandarasi feki waliokuwa kule Mwanga ukawafukuza, kwa sababu ungechelewa kuwafukuza, ningekufukuza mimi wewe,” amesema Dkt. Magufuli.

Amemruhusu waziri huyo ambaye amemsifu kuwa ameanza na kasi nzuri, kuwafukuza kazi wakandarasi wanaoshindwa kufanya kazi kwa ufanisi kwa sababu hawakuja kufanya mambo ya mchezo mchezo.

“Makandarasi ambao umewafukuza kwenye mradi, zungumza na Bodi ya Makandarasi kupitia Sheria Namba 17 ya Mwaka 1997 wafutwe wasipate kazi yoyote Tanzania nzima.”

Aidha, amesema kwa sababu Tanzania ina ushirikiano ndani Jumuiya ya Afrika Mashariki, basi majina ya wakandari hao yapelekwe huko ili pia watambulike. “Hatuhitaji makandarasi feki katika nchi hii.”

Baada ya kuzindua mradi huo leo mkoani Shinyanga, Januari 30, 2021, Rais Magufuli atazindua mradi wa maji wa Tabora – Igunga – Nzega ambao umetekelezwa kwa TZS bilioni 617.

Send this to a friend