Waziri wa Mambo ya Ndani apiga marufuku trafiki kujificha na kupiga tochi kwa kuvizia

0
57

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ameliagiza jeshi la polisi nchini kuwa na mbinu za kistaarabu za kisimamia sheria za usalama barabarani na kuacha kujificha na kuwashtukiza madereva wanaoendesha magari kwa mwendokasi.

George Simbachawene ameyasema hayo bungeni mjini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2020/2021, ambapo amesema vitendo vya polisi kujificha na kuvizia magari, vinaweza kupelekea wao wenyewe kugongwa.

“Kwanini tujifiche? Maana barabarani tupo kila siku, na sisi ndio madereva, sioni sababu ya kujificha. Spidi ziko barabarani mule, tuendelee kuongeza elimu zaidi kwa madereva wetu wapata uelewa na kufuata alama za barabarani,” amesisitiza Simbachawene.

Aidha, amemugiza IGP Simon Sirro kutoa maelekezo maalum juu ya udhibiti wa mwendo wa barabarani kwa sababu kinachofanyika sasa kinaleta fujo.

Ameongeza kuwa utaratibu wa polisi kutumia simu kupiga picha magari yanayokwenda kasi haukubaliki kwa sababu kuna kifaa maalum cha kufanya kazi hiyo.

“Huyu ana Nokia, huyu ana iPhone, huyu ana Samsung, tunaaminianaje, kwamba ni kitendea kazi ambacho tumekipitisha kisheria. Hii haikubali,” amesema.

Wakati huo huo, amesema kuwa kitendo cha polisi kusogeza picha iliyopigwa, ni jambo ambalo linahitaji msimamo wa kisheria kwani kama hakuna sheria inayotoa mamlaka hayo, mbinu hiyo haikubali kwa sababu inasema uongo, inawasingizia wengine na ndio sababu ya kuzuka kwa ubishi barabarani.

Send this to a friend