Waziri wa Mawasiliano Afrika Kusini ashutumiwa kwa kujaribu kubadilisha sheria ya umiliki kwa kampuni ya Elon Musk

0
10

Mwanasiasa mwandamizi wa Afrika Kusini amemtuhumu Waziri wa Mawasiliano, Solly Malatsi, kwa kujaribu kulegeza sheria za umiliki wa ndani za nchi hiyo ili kuvutia makampuni ya kigeni yanayotaka kufanya biashara nchini humo, ikiwa ni pamoja na Starlink ya Elon Musk.

Kwa mujibu wa Reuters, waziri huyo alitangaza mwaka jana kuwa atatoa mwelekeo wa sera ili kutambua programu ya usawa wa mtaji ndani ya sekta ya mawasiliano.

Hatua hiyo, alisema, inalenga kuongeza upatikanaji wa mtandao wa intaneti na kuwezesha makampuni ya kimataifa yanayopata ugumu wa kutimiza mahitaji ya umiliki wa ndani kufanya kazi Afrika Kusini.

Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki inataka kwamba makundi yaliyoachwa nyuma kwa miaka mingi (yaliyodhulumiwa kihistoria), lazima yamiliki angalau asilimia 30 ya hisa kwa mtoa leseni anayetaka kufanya kazi katika sekta za mawasiliano, utangazaji, au posta za Afrika Kusini.

Kampuni mama ya Starlink, SpaceX, iliandika barua kwa msimamizi wa mawasiliano wa Afrika Kusini, ICASA, ikisema kuwa sheria za umiliki wa ndani ni kikwazo kikubwa na kwamba inapaswa kufikiria tena mahitaji ya umiliki wa asilimia 30 kwa watoa leseni kwa kuanzisha programu ya usawa wa mtaji kama mbadala.