Waziri wa Watoto ajiuzulu kwa kuzaa na mvulana wa miaka 16

Waziri wa Watoto wa Iceland, Ásthildur Lóa Thórsdóttir (58) amejiuzulu baada ya kukiri kuwa alizaa mtoto na mvulana wa miaka 16 akiwa na miaka 23, miaka 30 iliyopita.
Kwa mujibu wa gazeti la Visir, Waziri huyo amewasilisha barua ya kujiuzulu alipoitwa kwenye ofisi ya Waziri Mkuu, ambaye ameeleza kupokea uthibitisho wa habari hiyo Alhamisi usiku. Hata hivyo, Thórsdóttir amesema hana mpango wa kuachia nafasi yake bungeni.
Taarifa zinaeleza kuwa Ásthildur alianza mahusiano na mvulana huyo akiwa na miaka 15 huku yeye akiwa na miaka 22 wakati akiwa mshauri katika kundi la kidini ambalo mvulana huyo alikuwa moja wa vijana waliokuwa wakihudhuria.
Ingawa umri unaoruhusiwa nchini Iceland ni miaka 15, ni kinyume cha sheria kushiriki ngono na mtu chini ya miaka 18 ikiwa wewe ni mwalimu, mshauri, au una mamlaka naye kifedha au kikazi.
Adhabu ya juu zaidi kwa kosa hilo ni kifungo cha miaka mitatu jela.