Wenye ulemavu Tanzania wanavyosafirishwa na kutumikishwa Kenya

0
16

Mkuu wa Kitengo cha Utafiti, Takwimu katika Sekretarieti ya Kupambana na biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu Tanzania, Alexander Lupilya amesema Serikali inatambua tatizo la usafirishaji haramu wa watoto na kwamba inachukua hatua mbalimbali kukabiliana nalo.

Amesema hayo kufuatia uchunguzi wa siri uliofanywa na BBC ulichofichua kisa cha walemavu wanaochukuliwa kutoka Tanzania mpaka nchini Kenya kisha kutumikishwa kuomba mitaani.

Aidha, amesema Serikali imesikitishwa kuona watoto wanasafirishwa hadi Kenya kwa ajili ya kutumikishwa, na sasa inawasiliana na mamlaka ya Kenya kutatua tatizo hilo.

“Mpaka sasa tuna wahanga watano wa biashara hiyo ambao wako Kenya wakisubiri kurejea Tanzania, hivyo tumekuwa tukiwasiliana na kufanya kazi kwa karibu na Serikali nchini Kenya,” amesema Lupilya.

Ameongeza kuwa hatua kadhaa zinachukuliwa ikiwa ni pamoja na kujenga uelewa ndani ya jamii ambapo wasafirishaji haramu huwarubuni waathiriwa, vilevile kutoa mafunzo kwa polisi na maafisa wa uhamiaji kutambua na kuchunguza visa kama hivyo.

Uchunguzi wa siri umebaini watoto wengi huchukuliwa kutoka kwa wazazi wao nchini Tanzania wakiahidiwa kupewa maisha bora, badala yake watoto wanalazimishwa kuomba mitaani na kuwanufaisha watekaji wao.

Send this to a friend