Wenye vibali wazuiwa kutumia maji ya Mto Ruvu kwa kilimo

0
54

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge amezuia vibali vya matumizi ya maji kutoka kwenye vyanzo vya maji kwenye Mto Ruvu na maeneo mengine ili kukabiliana na upungufu wa maji mkoani Dar es Salaam na Pwani.

Kunenge amesema hayo alipotembelea eneo la Kwa Dosa wilayani Kibaha na Kidogozero wilayani Bagamoyo kuangalia changamoto za baadhi ya watu kufanya kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia maji ya Mto Ruvu.

Alisema mkoa umeanzisha operesheni kupita maeneo yote ambayo wakulima wanatumia maji ya mto huo kwa ajili ya umwagiliaji ambapo wanatumia mashine kuvuta maji mtoni na hawaruhusiwi kufanya shughuli hizo hata kama wanavibali.

“Haturuhusu tena shughuli za kilimo kwa kipindi hichi hadi pale serikali itakapotoa maelekezo mengine, ila kwa sasa hilo haliruhusiwi. Hata kwa wale wenye vibali waache shughuli hizo mara moja kwenye maeneo yote yenye vyanzo maji,” amesema Kunenge.

Ofisa Msaidizi wa Bonde la Mto Wami-Ruvu, Halima Faraji amesema kuwa watu wanaolima kwenye eneo la Kwa Dosa hawana vibali vya kufanya shughuli hizo.

Faraji alisema wamekuwa wakizuia shughuli za kilimo au zozote wanapaswa kuwa umbali wa mita 60 kutoka kwenye mto lakini baadhi wamekuwa wakifanya ndani ya mita hizo.

Naye Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete ameeleza, eneo la kata ya Ruvu kuna mifugo mingi inayoingia kutoka mikoani baada ya kushushwa kwenye kituo cha kupumnzishia mifugo ili iendelee na safari lakini baadhi hawaipelekwi sehemu husika na kuiacha hapo na kuingia vijijini.