WhatsApp yaleta vigezo vipya vya lazima, wanaovikataa kuzuiwa kuitumia

0
22

Mtandao wa WhatsApp imewataka watumiaji wake, takribani bilioni mbili duniani kote, kukubali vigezo (terms) vipya vya kutumia programu hiyo, ambavyo vitaiwezesha programu hiyo kushirikishana (share) taarifa zaidi na kampuni mama, Facebook.

Aidha, maboresho yanajumuisha pia kuanzishwa kwa hudumu ya matangazo na ufanyaji biashara kwa njia ya mtandao (e-commerce).

Maboresho ya vigeo hivyo vimezua mkanganyiko miongoni mwa watumiaji wa mtandao huo unaohusisha kutumiana jumbe/taarifa za maneno, sauti, picha na video, kwani mtumiaji ambaye hatokubali vigezo hivyo, hatoweza kutumia WhatsApp kuanzia Februari 8, 2021 wakati vitakapoanza kutumika.

Facebook inakusudia kuitumia WhatsApp kibiashara kwa kuruhusu wafanyabiashara kuwasiliana na wateja wao na kuwauzia bidhaa moja kwa moja kama ambavyo tayari inafanyika nchini India.

Akizungumzia maboresho ya vigezo hivyo Msemaji wa Facebook amesema, “maboresho ya sera ya usiri na vigezo vya matumizi ni jambo la kawaida kwenye sekta hii, na tunawapatia watumiaji taarifa ya kutosha kupitia mabadiliko ambayo yataanza kutumika Februari 8.

Watumiaji wote wanatakiwa kukubali vigezo vipya vya huduma kama wanataka kuendelea kutumia WhatsApp,” ameongeza.

Kampuni hiyo imesema kuwa maboresho hayo yataruhusu kushirikishana taarifa kati ya WhatsApp na Facebook na programu zake nyingine kama vile Instagram na Messenger. Taarifa hizo ni kama mawasiliano (contacts) na taarifa za mtumiaji (profile data), lakini sio maudhui ya jumbe.

Ndani ya Umoja wa Ulaya (EU) na Uingereza maboresho haya yanahusu tu watumiaji wa WhatsApp Business.

Hata hivyo baadhi ya watu wamesema maboresho hayo si halali kwani kama njia pekee ya kuyakataa ni kuacha kitumia WhatsApp, basi ridhaa ya watumiaji inalazimishwa, kwa sababu matumizi ya taarifa binafsi za watu ni kosa.

Send this to a friend