WHO yaipa Tanzania Bilioni 7.5 kukabiliana na Virusi vya Marburg nchini

0
6

Rais Samia Suluhu Hassan amesema baada ya kuwepo kwa uvumi kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Marburg katika mkoa wa Kagera, vipimo vya maabara vimethibitisha mtu mmoja ameambukizwa virusi hivyo.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na vyombo vya Habari baada ya mkutano wake na Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus Ikulu jijini Dar es Salaam, ambapo amesema katika vipimo hivyo baadhi ya watu waliokuwa wakihisiwa kuwa na ugonjwa huo walithibitishwa kuwa na magonjwa mengine.

“Serikali ilichukua hatua za haraka ikiwemo uchunguzi wa watu waliotiliwa shaka, kuimarisha ufuatiliaji, na kuunda timu za dharura. Mnamo Januari 11, 2025, wataalamu walitumwa Kagera kuchunguza hali hiyo. Vipimo vya maabara vilithibitisha mgonjwa mmoja kuwa na virusi vya Marburg,” amesema Rais Samia.

Naye Mkurugenzi wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema shirika hilo limetoa Dola za Kimarekani milioni 3 [TZS Bilioni 7.5] kutoka kwenye Mfuko wa Dharura wa WHO ili kusaidia juhudi za kukabiliana na mlipuko wa Marburg nchini.

Aidha, amesema jitihada za serikali ya Tanzania katika kukabiliana na mlipuko uliopita mwaka 2023, umejenga uwezo ambao ana matumaini utawezesha Tanzania kudhibiti mlipuko huo wa sasa haraka iwezekanavyo.

 

 

Send this to a friend