Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa wito wa kuongezwa ushuru kwenye bidhaa za pombe na vinywaji vyenye sukari ili kupunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya vifo vitokanavyo na unywaji pombe pamoja na ulaji usiofaa.
WHO imesema kiwango cha wastani cha ushuru kimataifa kwenye bidhaa zinazohatarisha afya kilikuwa cha chini sana, huku ikisisitiza kuwa bidhaa kama vile mvinyo hazitozwi ushuru katika baadhi ya nchi za Ulaya.
Shirika hilo limesema kuongeza ushuru kutasaidia kupunguza matumizi ya bidhaa hizo na kutoa motisha kwa kampuni kutengeneza bidhaa zinazofaa kwa afya ya binaadamu.
Kulingana na takwimu ya WHO, watu milioni 2.6 hufariki kila mwaka kutokana na kunywa pombe huku watu milioni 8 wakifariki kutokana na ulaji usiofaa kila mwaka.
Aidha, utafiti wa 2017 unaonyesha ushuru unaoongeza bei ya pombe kwa asilimia 50 ungesaidia kuepusha zaidi ya vifo milioni 21 katika kipindi cha miaka 50 na kuzalisha karibu dola trilioni 17 katika mapato ya ziada.