Wizara ya Afya yatoa taarifa ongezeko la magonjwa ya mfumo wa hewa

0
41

Wizara ya Afya imesema takwimu za ufuatiliaji wa magonjwa ya mfumo wa hewa zinaonesha ongezeko la visa vya ugonjwa wa UVIKO- 19 kutoka visa 37 Oktoba, 2023 hadi visa 65 Desemba, 2023, sambamba na ongezeko la visa vya virusi vya mafua aina ya influenza kutoka visa 34 hadi 49 katika kipindi hicho.

Taarifa iliyotolewa na Wizara hiyo Desemba 13, 2023 imeeleza kuwa katika kipindi cha kuanzia Novemba 2023 kumekuwa na tetesi juu ya ongezeko la visa vya magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa sehemu mbalimbali hususani katika mkoa wa Dar es Salaam, hivyo wizara imekuwa ikifanya ufuatiliaji wa vimelea vinavyosababisha magonjwa hayo.

“Magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa yamekuwepo hapa nchini wakati wote. Aidha, kumekuwapo na vipindi vya kuongezeka na kupungua kwa visa hivi kwa vipindi tofauti katika mwaka.

Ugonjwa wa UVIKO-19 umeendelea kuwepo kwa kiwango cha chini kama magonjwa mengine ya mfumo wa njia ya hewa ukiongezeka na kupungua kwa nyakati tofauti za majira ya mwaka. Aidha, virusi vya Influenza vilivyobainika hapa nchini havina madhara makubwa, ndiyo sababu iliyopelekea kuitwa ugonjwa wa majira (seasonal Influenza),” imeeleza taarifa.

Send this to a friend