Wizara ya Afya yatoa ufafanuzi mzazi aliyedai kubadilishiwa mtoto hospitalini

0
6

Kufuatia taarifa iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu mama aliyejifungua kwa upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha kudai kubadilishiwa mtoto, Wizara ya Afya imemsimamisha kazi muuguzi aliyemhudumia ili kupisha uchunguzi.

Taarifa iliyotolewa na Wizara imesema mama huyo ambaye ni mkazi wa Daraja Mbili mkoani humo, Neema Kilugala amedai baada ya kujifungua Machi 24, mwaka huu alioneshwa mtoto wake na muuguzi akiwa mzima, na baadaye aligundua kuwa amebadilishiwa mtoto baada ya kuletewa akiwa amefungwa na vitenge ambavyo si vyake.

“Muuguzi wa hospitali hiyo alidai kuwa alichanganya vitenge vya mtoto mwingine, hivyo akaahidi kwenda kubadilisha, pamoja na kuchukua hatua hiyo bado kulikuwa na hali ya sintofahamu,” imeeleza taarifa ya Wizara.

Aidha, Wizara ya Afya imesema kwa kushirikiana na Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa na Jeshi la Polisi imechukua sampuli za wazazi waliojifungua kipindi hicho pamoja na za watoto kwa ajili ya uchunguzi wa vinasaba (DNA) katika ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Wizara ya Afya imesema baada ya uchunguzi kukamilika taarifa rasmi zitatolewa na hatua stahiki zitachukuliwa.