Wizara ya Elimu yazuia kuongezwa ada shule binafsi
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa maelekezo ya ulipaji wa ada kwa shule zisizo za serikali baada ya janga la corona kufuatia uwepo wa malalamiko kuhusu ulipaji wa ada na malipo mengine kwa shule za msingi na sekondari pindi zitakapofunguliwa Juni 29, 2020.
Wizara imeelekeza ada za shule zilipwe kulingana na makuliano yaliyofikiwa mwanzoni mwa mwaka wa masomo na kusiwepo na nyongeza yoyote katika kiwango cha ada.
Aidha, wizara imesema kuwa wazazi wanapaswa kuzingatia kuwa kiwango cha ada huwa kinakadiriwa kuzingatia gharama mbalimbali za uendeshaji wa shule, gharama ambazo ziliendelea kuwepo hata muda ambao shule zilikuwa zimefungwa, kama vile mishahara ya watumishi, ankara za umeme na maji n.k.
Kwa upande wa malipo ya chakula na usafiri, wizara imezielekeza kamati/bodi za ambazo ndizo zenye mamlaka ya kuendesha shule kufanya uchambuzi wa gharama inayopaswa kupungua kwa siku ambazo wanafunzi hawakuwa shuleni, na kwamba tathmini hii izingatie ratiba mpya ya mihula iliyotolewa na wizara.
Wizara imesisitiza kuwa kwa vile shule zilifungwa wakati muhula wa asomo ukiwa unaendelea, basi wanafunzi wote wapokelewe na kuendelea na masomo yao bila kikwazo chochote ili kukamilisha muhula huo.