
Rais Samia Suluhu Hassan ametoa pongezi kwa Wizara ya Maji kutokana na kasi ya utendaji wake katika sekta ya maji nchini na kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata maji safi na salama.
Akizungumza leo katika kilele cha Wiki ya Maji iliyokwenda sambamba na Uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Maji ya Mwaka 2002 Toleo la Mwaka 2025 katika Ukumbi wa Mlimani City amesema kutokana na umuhimu wa maji, Serikali inatenga bajeti kubwa ili wananchi waweze kufikiwa na huduma hiyo.
“Serikali tunafanya tunavyoweza, tunaweka bajeti ya kutosha maji yapatikane, mbali tu ya kumtua mama ndoo kichwani, lakini kulinda uhai na maendeleo ya taifa hili, kwa sababu bila maji taifa letu la Tanzania halina maana,” amesema.
Kuhusu hali ya upatikanaji wa maji, Rais Samia ameeleza mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya maji nchini, ambapo upatikanaji maji vijijini hadi sasa ni asilimia 83 ikiwa imebaki asilimia 2 kutimiza ahadi iliyotolewa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025. Vilevile, kwa mjini upatikanaji wa maji ni asilimia 95.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amemuagiza Waziri ya Maji, Jumaa Aweso kuanzisha Gridi ya Maji ya Taifa kama ilivyo Gridi ya Taifa ya Umeme akisema lengo ni kuwa na vituo vya kupokea maji kutoka vyanzo mbalimbali nchi nzima kwa kuweka vituo vya kanda kisha kuwa na utaratibu wa kusambaza maji nchi nzima.