Yanga yadai Simba ibabebwa Ligi Kuu

0
66

Klabu ya Soka ya Young Africans imeeleza kutoridhishwa na mwenendo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana na kuwemo makosa mbalimbali yanayofanywa na baadhi ya waamuzi.

Msemaji Mkuu Yanga, Hassan Bumbuli amesema baadhi ya waamuzi wamekuwa wakifanya vitendo ambavyo huwanyima haki baadhi ya timu na kuzinufaisha nyingine.

“Lengo letu ni kutaka waamuzi kujitafakari, pia tunataka mamlaka zinazosimamia mpira kuchukua hatua juu ya haya yanayoendelea ili kuipa thamani ligi na kuwapa thamani wale ambao wanawekeza katika mpira. Hali ya waamuzi kuamua kuwapa ushindi  wakina nani na nani wa kukataliwa si afya katika mpira, tunaweza kuhatarisha hali ya kiusalama,”amesema Bumbuli.

Hata hivyo Mhamasishaji wa Klabu hiyo, Haji Manara amesema kuwa, kumekuwa na upendeleo kwa baadhi ya timu  na uonevu katika utendaji haki hususani kwenye upande wa utoaji wa adhabu baina ya Simba na Young Africans.

“Mechi ya Simba na Kagera iliahirishwa kwa kuwa wachezaji wa Simba walikuwa wagonjwa. Mechi ya Yanga na Tanzania Prison ilikuwa ngumu kwetu, wachezaji wengi walikuwa wagonjwa lakini tukaambiwa hatujafuata utaratibu jinsi ya kuomba. Usiweke urafiki katika suala la haki za watu,” amesema Manara

Pia amewasihi waandishi wa habari na wachambuzi  kutojiingiza katika vitu vya ushabiki kwenye kazi zao badala yake wasimamie misingi na miiko ya taaluma zao.

Kwa sasa Young Africans inaongoza katika msimamo wa ligi ikiwa mbele kwa alama tano dhidi ya watani wao wa jadi Simba SC. Hata hivyo, Yanga ina mchezo mmoja dhidi ya wanajeshi wa mpakani Biashara United kutoka Mara.

Send this to a friend