Yanga yamfukuzisha kazi kocha wa Simba

0
26

Klabu ya Simba SC imevunja mkataba na kocha mkuu wa kikosi cha kwanza, Roberto Oliveira Goncalves Do Carmo (Robertinho) kwa makubaliano ya pande zote mbili pamoja na kufikia makubaliano ya kusitisha mkataba na kocha wa viungo, Corneille Hategekimana.

Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya Habari Novemba 07, 2023 imesema katika kipindi cha mpito, klabu hiyo itakuwa chini ya kocha Mhispania, Daniel Cadena akisaidiwa na Seleman Matola.

Simba amechukua uamuzi huo siku mbili baaada ya kupokea kipigo kizito cha 5-1 kutoka kwa wapinzani wao wa jadi, Yanga SC.

“Uongozi wa klabu ya Simba unawashukuru makocha hawa kwa mchango wao ndani ya klabu yetu na inawatakia kila la heri katika majukumu yao mapya,” imeeleza taarifa.

Aidha, uongozi huo umesema mchakato wa kutafuta makocha wapya tayari umeanza na unatarajiwa kukamilika hivi punde.

Robertinho alitinga klabuni hapo mwanzoni mwa Januari mwaka huu ambapo aliungana na Hategekimana raia wa Rwanda ambao waliwahi kufanya kazi pamoja wakiwa Rayon Sports.

Send this to a friend