Zaidi ya Dola Bilioni 2 zinahitajika Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia Afrika

0
84

Zaidi ya dola bilioni 2 kwa mwaka zinahitajika ili Bara la Afrika liweze kufanikisha Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia, hatua inayolenga kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, kulinda mazingira na kuboresha afya za wananchi.

Hayo yameelezwa pembezoni mwa Mkutano wa Pili wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika kuhusu Tabianchi uliofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia, ambapo viongozi na wadau mbalimbali wa nishati safi, akiwemo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Cosato Chumi, wamesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda na kimataifa.

Akifungua mjadala huo kwa niaba ya Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango, Cosato Chumi amesema ushirikiano katika uwekezaji, ufadhili wa masharti nafuu, ubunifu, teknolojia rafiki, kubadilishana uuzi na miundombinu ni msingi wa kutimiza malengo ya kitaifa na kimataifa.

Changamoto zitokanazo na matumizi ya nishati chafu zinaleta jitihada za pamoja za Serikali za Afrika, taasisi za kifedha, mashirika binafsi na wafadhili kutafuta zaidi ya dola bilioni mbili kila mwaka zitakazochangia kuleta suluhu.

Aidha, washiriki wa mjadala huo wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa jitihada za nishati safi ya kupikia. Mkakati wa Tanzania katika kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034 unajumuisha matumizi ya umeme, gesi asilia, LPG, teknolojia za upepo, jua na biomasi bunifu, hatua inayolenga kuboresha afya, kulinda mazingira na kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.

Send this to a friend