Zambia na Falme za Kiarabu zasaini makubaliano ya uchimbaji madini

0
39

Zambia imesaini makubaliano kadhaa ya ushirikiano na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) katika hafla iliyofanyika Ikulu ya nchi hiyo na kuhudhuriwa na Waziri wa Nchi wa Mambo ya Nje wa UAE, Sheikh Shakhboot Bin Nahyan Al Nahyan pamoja na ujumbe wake.

Viongozi hao wakiongozwa na mwenyeji wao, Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, wametia saini makubaliano ya ushirikiano katika maeneo muhimu kama uchimbaji madini, biashara ndogo na za kati (SMEs), na teknolojia ya dijiti.

Rais Hichilema ametoa shukrani zake kwa Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan, Rais wa Falme za Kiarabu kwa kuruhusu ujumbe huo kutembelea nchi yake na kusisitiza kuwa Zambia ina lengo la kujifunza kutokana na uzoefu wa mafanikio ya kiuchumi ya Falme za Kiarabu na kutumia maarifa hayo kuimarisha maendeleo katika nchi yake.

Katika hatua nyingine, Zambia imeshirikiana na kampuni ya ACSG Westland Consortium katika uwekezaji wa mradi mkubwa wa nishati utakaozalisha megawati 500 + 10MW utakaotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini humo.

Moja ya malengo makubwa ya ushirikiano huo ni kuwezesha ukuaji wa uchumi na ustawi kwa wananchi wa Zambia. Uwekezaji katika sekta ya nishati ni miongoni mwa maeneo muhimu ambayo serikali ya Zambia inalenga kuboresha

Mwenyekiti Mtendaji wa ACSG Westland Consortium, Bwana Obi Amuchienwa, ameeleza furaha yake kwa kushiriki katika uwekezaji huo mkubwa wa sekta ya nishati kwa kusema, “Tunafurahi kuwa sehemu ya juhudi za kuleta uhakika wa nishati kwa nchi hii na kuwa na ziada ya kusafirisha kwenye kanda.”

Rais Hichilema ameipongeza kampuni hiyo kwa uwekezaji huo mkubwa na kuahidi kuwa serikali itafanya kila juhudi kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi ili kutatua upungufu wa umeme katika maeneo ya mbali ambayo pia yanaweza kuwa maeneo yenye uwezo wa kiuchumi.

Send this to a friend