Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetenga shilingi Bilioni 34 kwa ajili ya posho ya nauli kwa wafanyakazi ambapo kila mtumishi atapewa shilingi elfu hamsini ili kuchochea ufanisi wa kazi.
Akizungumza katika sherehe za Siku ya Wafanyakazi ‘Mei Mosi’ zilizofanyika katika Uwanja wa Gombani Mkoa wa Kusini Pemba Rais Dkt. Hussein Mwinyi amesema Serikali itachukua hatua za kuanza kutoa posho ya nauli za kwenda kazini na kurudi kwa watumishi wanaostahiki kulipwa posho.
Ameongeza kuwa Serikali imedhamiria kuhakikisha inaongeza fedha kwa ajili ya posho ya likizo, zikiwa zimetengwa shilingi Bilioni 2.5 katika bajeti mpya mwaka 2024/2025.
Aidha, Dkt. Mwinyi amesema katika kipindi cha miaka mitano, Serikali imepanga kutengeneza ajira 300,000 kwa wananchi na kwamba tayari Serikali kupitia shughuli mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya maendeleo, imefanikisha upatikanaji wa ajira 180,000.