Zanzibar kuwapa hifadhi watalii 900 waliokwama kurudi Ukraine

0
39

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi amesema wameanza  mazungumzo na wamiliki wa hoteli kutoka Zanzibar kuona jinsi gani ya kuwasaidia watalii kutoka Ukraine waliokwama visiwani hapo.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari na wanahabari kama ambavyo hufanya kila mwisho wa mwezi amesema kuna watalii takribani 900 wako visiwani Zanzibar ambao wameshindwa kurudi nchini kwao kutokana na vita inayoendelea nchini humo.

Watalii hao wameomba msaada kwa Serikali iwasaidie sehemu ya makazi kwa kipindi hiki, kwa kuwa wameishiwa fedha za kujikimu na hawawezi kumudu gharama za hoteli. 

Hivyo, Rais wa Zanzibar amesema wanazungumza na wamiliki wa hoteli na namna watakavyoweza  kuwapa msaada bila kuchajiwa mpaka pale Serikali ya Ukraine itakapoleta msaada.

“Tunaangalia namna ya kuwasaidia mpaka serikali yao itakapopata uwezo wa kuleta msaada. Lakini pia Serikali kuwaangalia wale wenye Hoteli kwa upande wa kodi, kwahiyo tunazungumza, ukweli ni kwamba tunaona umuhimu wa kutoa msaada” amesema Rais Hussein.

Hata hivyo, Waziri wa Utalii wa Zanzibar Leila Mohammed amesema Watalii hao tayari wanaendelea kupewa huduma za kibinadamu licha ya wengine kumaliza siku zao za kitalii.

Ni siku ya tano sasa nchi ya Ukraine iko katika vita dhidi ya Urusi huku maelfu ya watu wakiripotiwa kuuawa, na waathirika wengi wakiwa wanawake  wazee na watoto.

Send this to a friend