
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky amesema anaamini zaidi ya wanajeshi 46,000 wa nchi hiyo wameuawa na wengine takriban 380,000 wamejeruhiwa tangu kuanza kwa vita dhidi ya Urusi February 24, 2022.
Zelensky amekadiria pia kuwa makumi ya maelfu ya raia wa Ukraine wameuawa huku watoto takriban 20,000 wakihamishwa kwa nguvu kwenda Urusi.
“Tunao zaidi ya wanajeshi 46,000 waliouawa.Ni vigumu kusema, makumi ya maelfu zaidi ambao hawajulikani walipo au wako matekani na huwezi kujua kwa uhakika kwa sababu waliopotea vitani huenda wakawa wamekufa,” amesema.
Ameongeza kuwa “Nadhani kuna takriban 380,000 waliojeruhiwa, na kuna watoto 20,000 waliohamishwa kwa nguvu kwenda Urusi.”
Zelensky amesema Ukraine mara nyingi imekuwa ikichukua tahadhari zaidi kutoa takwimu za vifo kwa kuhofia kwamba huenda zikadhoofisha morali ya nchi hiyo.