Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kukutana na Rais wa Jamhuri ya Guinea-Bissau na Mwenyekiti wa Taasisi ya Muungano wa Viongozi wa Afrika katika Kudhibiti Malaria (ALMA), Umaro Sissoco Embaló anayetarajiwa kuwasili nchini kwa ziara ya siku tatu na kujadili masuala ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara, Balozi Samwel Shelukindo amesema ujio wa Rais Embaló wa Guinea-Bissau utazalisha fursa za uwekezaji na ushirikiano kibiashara katika matumizi mazuri ya Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) ambapo nchi zote mbili zimeridhia uanzishwaji wake.
Watanzania wanaojihusisha na uzalishaji na uchakataji wa bidhaa za korosho nao watanufaika kwani Guinea-Bissau ni wazalishaji wazuri wa zao la Korosho.
Mbali na kufanya mazungumzo na mweneyji wake, Rais Samia Suluhu, Rais Embaló atatembelea pia Taasisi ya ALMA, Miundombinu ya Reli ya Kisasa (SGR) katika Kituo cha Stesheni jijini Dar es Salaam pamoja na Mamlaka ya Eneo Huru la Uwekezaji kwa Mauzo Nje (EPZA).
Rais Embaló atawasili Tanzania hapo kesho Juni 21, 2024 ambapo atapokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba (Mb.) na mapokezi rasmi kufanyika Ikulu Juni 22, 2024.