Zifahamu sababu 3 zinazomfanya CAG kuondolewa kabla ya muda wake kumalizika
Moja na mijadala inayoendelea kujadiliwa kwa wingi kwenye mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari ni kauli ya aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad kueleza kuwa kulikuwa na uvunjwaji wa katiba katika kumwondoa kwenye ofisi hiyo.
Prof. Assad alisema hayo jijini Dodoma Oktoba 6, 2021 wakati wa mdahalo juu ya kitabu cha Rai ya Jenerali kinachozungumzia umuhimu wa Katiba Mpya, akisema kuwa “Sipendi sana kusikia neno mstaafu na kwamba neno hilo linaniudhi linapotamkwa mbele yangu.”
Aliteuliwa na aliyekuwa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kuwa CAG Novemba 5, 2014 na alitoka kwenye nafasi hiyo Novemba 4, 2019 kwa maelezo kuwa alimaliza muda wake.
Je! Katiba ya Tanzania inatoa maelezo gani kuhusu kumwondoa CAG kwenye ofisi hiyo? Ibara ya 144 (1-5) inaeleza mazingira ambayo yanaweza kupelekea CAG kuondolewa ikiwa ni;
(1) Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu wa Jamhuri ya Muungano atalazimika kuacha kazi yake atakapotimiza umri wa miaka sitini au umri mwingine wowote utakaotajwa na Sheria iliyotungwa na Bunge.
(2) Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu aweza tu kuondolewa katika madaraka ya kazi yake kwa sababu ya kushindwa kutekeleza kazi zake (ama kutokana na maradhi au sababu nyingine yoyote) au kwa sababu ya tabia mbaya, au kwa kuvunja masharti ya sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na hataweza kuondolewa kazini ila kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (4) ya ibara hii.
(3) Iwapo Rais anaona kwamba suala la kumwondoa kazini Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu kwa mujibu wa masharti ya ibara hii lahitaji kuchunguzwa, basi katika hali hiyo mambo yatakuwa ifuatavyo:
(a) Rais atateua Tume Maalum ambayo itakuwa na Mwenyekiti na Wajumbe wengine wasiopungua wawili. Huyo Mwenyekiti na angalau nusu ya wajumbe wengine wa Tume hiyo itabidi wawe watu ambao ni Majaji au watu waliopata kuwa Majaji wa Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani katika nchi yoyote iliyomo kwenye Jumuiya ya Madola;
(b) Tume hiyo itachunguza shauri lote halafu itatoa taarifa kwa Rais kuhusu maelezo ya shauri lote na itamshauri Rais kama huyo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu aondolewe kazini kwa mujibu wa masharti ya ibara hii kwa sababu ya kushindwa kufanya kazi kutokana na maradhi au sababu nyingine yoyote au kwa sababu ya tabia mbaya.
(4) Ikiwa Tume iliyoteuliwa kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (3) itamshauri Rais kwamba huyo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu aondolewe kazini kwa sababu ya kushindwa kufanya kazi kutokana na maradhi au sababu nyingine yoyote au kwa sababu ya tabia mbaya, basi Rais atamwondoa kazini.
(5) Ikiwa suala la kumwondoa kazini Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu limepelekwa kwenye Tume kwa ajili ya uchunguzi kwa mujibu wa masharti ya ibara hii, Rais aweza kumsimamisha kazi huyo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu, na Rais aweza wakati wowote kufuta uamuzi huo wa kumsimamisha kazi, na kwa hali yoyote uamuzi huo utabatilika ikiwa Tume itamshauri Rais kwamba huyo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu asiondolewe kazini.
Aidha, kwa mujibu waSheria ya Ukaguzi wa Umma ya Mwaka 2008, CAG atashika ofisi kwa kipindi cha miaka mitano, na ataweza kuongeza kwa kipindi kingine kimoja tu.
Sheria hiyo inaeleza zaidi kwamba CAG ataondolewa katika ofisi hiyo endapo atajiuzulu kutokana na sababu za kiafya au sababu nyingine ambayo Rais ataona kuwa inajitosheleza. Katika hili la kujiuzulu, CAG atatakiwa kutoa notisi ya miezi sita kwa Rais.