Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amewasihi wanasiasa na Watanzania kujenga mshikamano na Rais Samia Suluhu Hassan na kumpa moyo ili kufanikisha hatua ya utekelezaji wa mageuzi ya kisheria na kikatiba.
Akiandika kupitia ukurasa wake wa Twitter, Zitto amesema chama chake kiliona dhamira ya Rais Samia Suluhu ya kuboresha mazingira ya siasa nchini, hivyo kiliamua kumuunga mkono kufuatia hotuba ya kiapo na hotuba zake bungeni, mikutano mbalimbali na wadau ikiwemo mkutano wa TCD, Dodoma.
Afisa upelelezi akamatwa akidaiwa kuwaachia huru watuhumiwa
Zitto ameongeza kuwa chama chake kilimuunga mkono kwa sababu kiliona uungwana na nia yake thabiti kama kiongozi na kukataa kukaa upande wa kumkatisha tamaa, hivyo kushiriki kikosi kazi kikamilifu.
“Tulitukanwa, tulibezwa, tulikashifiwa, hatukujali. Sasa Kikosi kazi kimekamilisha taarifa, na hivi karibuni itawasilisha kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ushauri wangu kwa wanasiasa wenzangu: Jivueni minyororo ya 2020. Hairudi tena, mageuzi yanahitaji mshikamano,” ameandika Zitto Kabwe.