in

Rais Samia aiomba Benki ya Maendeleo ya Afrika kuongeza idadi ya Watanzania inaowaajiri

Rais Samia Suluhu Hassan amemwomba Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Adesina Akinumwi kuongeza nafasi za Watanzania wanaoajiriwa katika benki hiyo.

Rais Samia ametoa ombi hilo wakati akizungumza kwa njia simu na Akinumwi kuhusu uhusiano wa Tanzania na benki hiyo ambayo imekuwa ikifadhili miradi mbalimbali ya maendeleo.

Akinumwi ameahidi kuwa AfDB itatoa ufadhili kwa Tanzania ili kuanzisha benki za wajasiriamali zitakazowakopesha vijana wanaohitimu mafunzo ya ufundi stadi pamoja na kujihusisha na kilimo, jambo litakalosaidia kupungua kwa tatizo la ajira kwa vijana na kuwaongezea kipato.

Aidha, Dkt. Adesina amemualika Mhe. Rais Samia kuhudhuria mkutano wa uwekezaji utakaowaleta wawekezaji wakubwa pamoja ambao unatarajiwa kuvutia mabilioni ya fedha kwa ajili ya kuwekeza katika nchi mbalimbali.

Pia, Dkt. Adesina amesema AfDB imetenga dola za Marekani Bilioni 5 kwa ajili ya kusaidia wanawake na ameomba Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa uwezeshaji wanawake kiuchumi ambapo Mhe. Rais Samia amekubali ombi hilo.

Kwa upande wake Rais Samia ameelezea kufurahishwa kwake na mradi wa AfDB wa kufadhili vijana wanaojihusisha na kilimo na wanaomaliza mafunzo katika vyuo vya ufundi stadi kwa kuwa ufadhili huo utawawezesha vijana wengi wa Tanzania kuzalisha mali.

34,000 wapandishwa vyeo Mambo ya Ndani

Serikali kuja na mpango wa kuirejesha Tanzanite Tanzania