in ,

Msimamo wa Serikali kuhusu utekelezaji wa kitita kipya cha NHIF

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ametoa rai kwa hospitali zote zilizositisha kutoa huduma kwa wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima Afya (NHIF) kuendelea kuwahudumia wanachama hao na kutowaondoa wodini wagonjwa wanaopata huduma kwani kwa kufanya hivyo ni kuvunja sheria.

Taarifa iliyotolewa na Waziri Ummy imefafanua kuwa wizara iliamua kusitisha utekelezaji wa kitita kipya cha NHIF baada ya kusikiliza hoja za wadau na hoja za NHIF mwezi Januari, na kuunda kamati ya wataalam kutoka Serikalini, sekta binafsi na taasisi za bima kwa ajili ya kuishauri Serikali kuhusu hoja za APHFTA na NHIF, pia kufanya mapitio ya bei na kuandaa vigezo vinavyopaswa kuzingatiwa katika maboresho ya kitita hicho bila kuathiri upande wowote.

Amesema baada ya kukamilisha jukumu hilo Februari 19, 2024 kamati iliwasilisha taarifa yake wizarani katika kikao kilichoshirikisha wadau wote ikiwemo APHFTA, CSSC, BAKWATA, TIRA, Chama cha Madaktari Tanzania na NHIF. Taarifa hiyo pia iliwasilishwa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI ili kupata maoni na ushauri kabla ya utekelezaji na baada ya kupokea maoni Wizara ilielekeza NHIF kuanza utekelezaji wa kitita kipya cha mwaka 2023.

“Licha ya ushirikishwaji mkubwa uliofanyika katika mchakato mzima wa maboresho ya Kitita cha Mafao cha NHIF cha mwaka 2023, Wizara imepokea kwa masikitiko makubwa namna ambavyo baadhi ya watoa huduma wameamua kusitisha huduma licha ya kupewa fursa ya kuwasilisha maoni na ushauri wao kuhusu suala hili,” amesema.

Aidha, ameiagiza Kamati ya kitaalamu iendelee kufanya majadiliano na watoa huduma wakati huduma zikiendelea kutolewa pamoja na hospitali zote za Serikali nchini kujiandaa na kuweka utaratibu mzuri wa kuwapokea wagonjwa wengi zaidi na kuwahudumia kwa weledi wa hali ya juu hasa katika kipindi hiki.

Mbali na hayo, Waziri amemwelekeza Msajili wa Hospitali Binafsi kutoa notisi na kuchukua hatua mara moja kwa watoa huduma wote ambao kwa namna moja watakiuka sheria anazozisimamia.

Bunge la Ghana lakatiwa umeme kwa kutolipa deni

Muhimbili yaja na mpango wa dharura kuhudumia wanachama wa NHIF