Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) umesema Hospitali hiyo imeongeza muda wa kuona wagonjwa katika kliniki zote za Upanga kupitia vyumba 75 vya kuona wagonjwa na vyumba vya kuona wagonjwa 59 vilivyopo Mloganzila kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa nne usiku au mpaka mgonjwa wa mwisho atakapomaliza kuonwa na daktari.
Hatua hiyo ni kufuatia baadhi ya Hospitali kusitisha huduma kwa wanachama wa Mfuko wa NHIF kuanzia Machi 1, 2024 kutokana na kile walichosema kuwa kitita hicho hakiendani na uhalisia wa soko.
Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Mohamed Janabi amesema hospitali hiyo imefanikiwa kuhamia kwenye kitita kipya cha mafao cha mwaka 2023 kilichopendekezwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ambapo huduma zinaendelea kutolewa.
Msimamo wa Serikali kuhusu utekelezaji wa kitita kipya cha NHIF
“Tunajua kuna wagonjwa waliopangwa kufanyiwa upasuaji, tunavyo vyumba 18 vya upasuaji Upanga na Mloganzila vyumba vya upasuaji 13. Kwa wagonjwa wenye tatizo la figo wanaohitaji kusafishwa damu, Upanga tunazo mashine 47 za kutoa huduma hiyo na tumeongeza zamu za kutoa huduma hiyo katika mzunguko wa saa nne wa kila zamu kutoka tatu hadi nne kwa Upanga na Mloganzila ambapo kuna mashine 12 tumeongezea mizunguko kutoka miwili hadi minne,” ameeleza.
Aidha, Prof. Janabi amesema MNH kama mmoja wa watoa huduma wakubwa nchini, itaendelea kufuatilia utendaji wa kitita hicho ili kubaini changamoto zitakazojitokeza na kuziwasilisha katika mamlaka husika.