in

Bashungwa aagiza mkandarasi aondolewe kwa kukosa vigezo

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, ameuagiza Wakala wa Barabara (TANROADS) kumuondoa mkandarasi wa kampuni ya Kay Bouvet Engineering Ltd ya nchini India na kumtafuta mkandarasi mwingine mwenye uwezo na sifa za kujenga miundombinu ya barabara katika kiwanda cha sukari cha Mkulazi mkoani Morogoro.

Ameeleza hayo wakati akikagua ujenzi wa kiwanda na miundombinu ya barabara katika Kiwanda cha Sukari na Shamba la Mbigiri ambapo amebaini mkandarasi huyo hana sifa za kutekeleza mradi huo.

“Jukumu la TANROADS ni kusimamia ujenzi wa kiwanda hiki katika miundombinu ya barabara, lakini Mkandarasi huyu ni mbabaishaji, na tumeamua kumuondoa kwa kuwa hana mitambo ya kutosha ya kutekeleza kazi ya ujenzi wa barabara, pia hana sifa na uzoefu wa barabara kwa kiwango cha lami”, amesema Bashungwa.

Aidha, Bashungwa amesema kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu ya kiwanda hicho kilichofikia asilimia 70 kutasaidia kuongeza uzalishaji wa sukari nchini na kulisaidia Taifa kuzalisha sukari ya kujitosheleza kupitia viwanda vya ndani.

Akitoa taarifa ya mradi huo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Alinanuswe Kyamba amesema TANROADS ina jukumu la kusimamia kazi zote za manunuzi, ujenzi wa kiwanda, majaribio na shughuli zote za ukamilishaji wa kiwanda na kuanza uzalishaji wa sukari katika kiwanda hicho cha Mkulazi.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, amesema Mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa miundombinu ya barabara amekuwa akisuasua na kupelekea shughuli za uzalishaji wa kiwanda hicho kutokufanyika kwa ufanisi kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara zinazounganisha kiwanda na mashamba ya miwa.

Serikali yatangaza kuwasajili madalali wa mazao

Uganda: Mahakama yatoa adhabu kwa wanawake wanaotuma watoto kuomba mtaani