in , ,

Mjamzito afariki kwa kuongezewa damu kimakosa mkoani Tanga

Watumishi watano wa Kituo cha Afya Mikanjuni wamesimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi baada ya kudaiwa kufanya uzembe na kusababisha kifo cha mjamzito, Fatuma Mussa Suleiman (36) mkazi wa Magaoni jijini Tanga aliyefika kituoni hapo kwa ajili ya kujifungua.

Imeelezwa kuwa mjamzito huyo aliwekewa damu ambayo hakustahili kuwekewa na wala hakuwa na uhitaji nayo, kitendo kilichochukuliwa kuwa ni uzembe wa hali ya juu uliofanywa na wahudumu wa zamu.

Mkuu wa Wilaya ya Tanga, James Kaji amesema baada ya kutokea uzembe huo, marehemu alipata uzio mkali (Allergic Reaction) na hivyo kupelekea kifo chake.

“Mgonjwa alifanyiwa upasuaji ambapo alifanikiwa kupata mtoto wa kike na hakukuwa na changamoto yoyote kwa mama wala kwa mtoto baada ya upasuaji na aliendelea na matibabu chini ya uangalizi wa madaktari na wauguzi wa zamu.”

“Katika wodi hiyo alipolazwa kulikuwa na mgonjwa ambaye alikuwa na uhitaji wa kuwekewa damu na ilikuwa tayari imeandaliwa, kwa hiyo muuguzi aliyekuwa zamu alimwekea damu marehemu badala ya mgonjwa aliyekuwa anatakiwa kuwekewa damu,” amesema DC Kaji.

Watumishi waliosimamishwa kazi ni pamoja na wauguzi watatu ambao ni Fadhila Ally Hoza, Restituta Kasendo Deusdedit, pamoja na Muya Ally Mhando ambapo kwa upande wa madaktari ni Hamis Mohamed Msami pamoja na Andrew Eliasikia Kidee.

Serikali ya Zanzibar yalaani unyanyasaji unaofanyika kwa sababu za kidini

Rais Samia afanya uteuzi, utenguzi na uhamisho wa viongozi mbalimbali