in ,

DART yawasimamisha kazi watumishi kisa vurugu za abiria na madereva Kivukoni

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) imewasimamisha kazi watumishi akiwemo Msimamizi wa Kituo cha Kivukoni, Shabani Kajiru, Afisa Ufuatiliaji wa Kituo, Brown Mlawa pamoja na kumwelekeza mtoa huduma wa mpito (UDART) kuwasimamisha kazi madereva wawili, Salehe Maziku na Chande Likotimo na msimamizi wa kituo hicho, Eric Mukaro kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Hatua hiyo ni imekuja baada ya kutokea kwa vurugu kati ya abiria na madereva wa basi la mwendokasi lililokuwa linafanya safari kutoka Kivukoni – Morocco katika eneo la Kivukoni kwenye kituo cha Mwendokasi majira ya saa 2 usiku, Machi 26, 2024.

Kwa mujibu wa DART, vurugu hizo zilitokea baada ya abiria wengi waliokuwa wakisubiri gari la kwenda Kimara kwa muda mrefu kuamua kuingia kwenye basi hilo na kumwamrisha dereva wa basi akiwa na mwenzake kuwapeleka Kimara hali ambayo hawakukubaliana nayo na hivyo kusababisha vurugu kati yao huku madereva wakiamua kuwapeleka Morocco.

“Baada ya malumbano ya muda mrefu madereva wakaamua kuwarudisha abiria hao Kivukoni kitu ambacho sio busara kutokana na hali iliyokuwepo, na malumbano yalipozidi ndipo walipoamua kuwapeleka abiria hao Kimara,” imesema DART.

Aidha, DART imetoa onyo kwa watumishi wake kuwa haitosita kuchukua hatua za haraka kwa watumishi watakaokiuka maadili ya utoaji wa huduma kwa wananchi pamoja na kuomba radhi kwa kitendo kilichotokea.

NMB yafuturisha Dar, Waziri Mkuu azitaka Serikali za Mitaa, Taasisi zijifunze kwao

Rais Samia: Ripoti za CAG zinaimarisha utendaji serikalini