in , ,

Mabeyo: Hayati Magufuli alitaka kurudishwa nyumbani kabla ya kufariki

Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Jenerali Venance Mabeyo ameeleza kuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Pombe Magufuli alitaka arudishwe nyumbani kutoka hospitalini, baada ya kuona hawezi kupona ili afariki akiwa nyumbani.

Ameyasema hayo katika mahojiano maalumu na Daily News Digital, ikiwa ni kumbukizi ya miaka mitatu ya kifo cha Rais Dkt. Magufuli kilichotokea Machi 17, 2021 katika hospitali ya Kumbukumbu ya Emilio Mzena mkoani Dar es Salaam alikokuwa akitibiwa maradhi ya moyo.

“Mwenyezi Mungu alimwongoza kwamba hatapona, alichosema nirudisheni nyumbani nikafie nyumbani, tukasema Mheshimiwa hapana, hapa uko kwenye mikono salama, madaktari wapo waendelee kukutibu,” ameeleza Mabeyo.

Ameongeza, “Aliniita, CDF njoo, akaniambia siwezi kupona, waamuru hawa madaktari wanirudishe nyumbani. Nikamwambia Mheshimiwa sina mamlaka hayo,” ameeleza Jenerali Mabeyo.

Katika simulizi ya kifo cha Hayati Magufuli, Jenerali Mabeyo ameeleza jinsi walivyopata ugumu kuamua iwapo Rais ambaye alikuwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu aapishwe kabla ya mazishi au baada ya mazishi, ambapo kwa pamoja walifikia makubaliano ya kumuapisha kabla ya mazishi ili marais wengine ambao wangeshiriki mazishi hayo wapokelewe na Rais.

Amesema kiutaratibu Rais mpya alipaswa kuapishwa ndani ya saa 24, lakini aliapishwa baada ya siku mbili kutokana na mijadala hiyo ikiwemo endapo kuwepo na sherehe za uapisho au zisiwepo.

Aidha, ameeleza kuwa katika hatua ya kumuapisha Rais Samia Suluhu ambaye ndiye amekuwa Rais wa kwanza mwanamke nchini, kulikuwa na mijadala iwapo Rais aitwe Amirati badala ya Amiri Jeshi, ambapo alieleza kuwa jeshi halitambui mwanamke au mwanaume, hivyo Amiri Jeshi hawezi kuitwa Amirati.

DRC yaishtaki Rwanda Mahakama ya Afrika Mashariki

TBS yasema vyakula vilivyotolewa na Marekani ni salama